Huku Taifa likijiandaa na mashindano ya Umoja wa Michezo kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISETA) yatakayoanza rasmi kesho tarehe 19 Juni 2025 mkoani Iringa, Halmashauri ya Wilaya ya Songea imeendelea kung’ara kama chachu ya maendeleo ya michezo kwa wanafunzi baada ya kutoa idadi kubwa ya wachezaji watakaoiwakilisha timu ya Mkoa wa Ruvuma.
Akizungumzia maandalizi ya mashindano hayo, Afisa Michezo wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Ndugu Francis Shuka, amesema “maandalizi yamekamilika na timu ya wanamichezo ipo njiani kuelekea Iringa huku viongozi wa msafara wakiwa tayari wamewasili kwa ajili ya maandalizi ya mwisho.
"Timu yetu imejiandaa kikamilifu na tunajivunia kutoa mchango mkubwa katika timu ya Mkoa, hususan katika mchezo wa pete ambapo tumetoa wachezaji 5 sawa na nusu ya timu nzima. Hii ni dhihirisho la juhudi zetu katika kukuza michezo mashuleni," amesema Shuka.
Mbali na mchezo wa pete, Halmashauri ya Wilaya ya Songea pia imetoa wachezaji 4 wa mpira wa miguu wa kiume, wachezaji 4 wa mpira wa miguu wa kike, pamoja na wachezaji 2 wa mpira wa kikapu kwa upande wa wanawake hali inayodhihirisha kuwa vipaji vinaibuliwa kwa jinsia zote na katika michezo tofauti tofauti.
Katika hatua nyingine ya kuonyesha mshikamano na ushirikiano, Ndg. Shuka amewashukuru wazazi na walezi kwa kuwa mabalozi wazuri wa maendeleo ya michezo kwa watoto wao. Ameeleza kuwa uelewa wao juu ya umuhimu wa michezo katika makuzi ya wanafunzi umechangia mafanikio haya.
Aidha, ametoa wito mahsusi kwa wakuu wa shule kuendelea kutenga nafasi kwa wanafunzi wenye vipaji vya michezo, akisisitiza kuwa michezo si kikwazo cha taaluma, bali ni nyenzo muhimu ya kuinua ari ya kujifunza na nidhamu kwa vijana.
Katika hotuba yake, Shuka alimshukuru kwa dhati Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Bi Elizabeth Gumbo, kwa kuwa mstari wa mbele katika kusapoti jitihada za michezo. Vilevile alitoa shukrani kwa Idara ya Elimu, ikijumuisha elimu msingi na sekondari, kwa kushirikiana bega kwa bega katika kufanikisha safari hii.
Kwa mafanikio haya, Halmashauri ya Wilaya ya Songea imeendelea kuthibitisha kuwa ni kitovu cha vipaji na mfano wa kuigwa kitaifa, si tu katika taaluma bali pia katika kuinua michezo mashuleni. Mashindano hayo yamebeba kauli mbiu isemayo Viongozi Bora ni msingi wa Maendeleo ya Taaluma, Sanaa na Michezo, Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa Amani na Utulivu
Halmashauri ya Wilaya Songea
Anuani ya Posta: P.o.box 995, Songea
Simu: 2602320 / 2602176
Simu ya mkononi:
Barua pepe: dedsongea@songeadc.go.tz
Copyright ©2017 songeadc.go.tz. Haki imehifadhiwa